Makumbusho haya ni mahali pa hadithi. Hadithi kuhusu Iringa ilivyokuwa zamani na sasa. Hadithi kuhusu watu mbalimbali wanaoifanya Iringa kuwa maskani yao. Hadithi kuhusu mila, desturi na mifumo ya maisha. Na hadithi kuhusu maeneo ya kuvutia ambayo huifanya Iringa kuwa ya kipekee.
Iringa Boma ni moja ya majengo ya zamani yaliyosalia katika mji wa Iringa. Boma hili lilijengwa katika miaka ya 1900 na utawala wa kikoloni wa kijerumani ambapo lilitumika kama hospitali ya kijeshi. Wasanifu wa kikoloni wa kijerumani walisanifu jengo hili kwa mchanganyiko wa mtindo wa kiafrika, kiswahili na kimagharibi. Baada ya Vita Kuu ya pili ya Dunia, waingereza walilifanya jengo hili kama kituo cha utawala cha kikanda. Toka Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961 hadi 2014, Iringa Boma iliendelea kutumika kama jengo la utawala wa kikanda na baadae kuwa ofisi ya kiutawala ya wilaya.
Kuanzia mwaka 2014 jengo hili lilikarabatiwa na kurejeshwa katika uhalisia wake ikiwa ni sehemu ya mradi wa fahari yetu chini ya Chuo Kikuu cha Iringa. Baada ya kufunguliwa mwaka 2016, Iringa Boma sasa inafanya kazi kama Makumbusho ya Mkoa na kituo cha utamaduni.