Chuo Kikuu cha Iringa (Uol)

Ni chuo kikuu binafsi kilichopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Chuo kina wanafunzi takriban 4000 ambao wamesajiliwa katika vitivo vya Sanaa na Sayansi ya jamii, Biashara na Uchumi, Ushauri nasaha na Saikolojia. Vitivo vingine ni Sheria Sayansi na Elimu na Theolojia. Mradi wa Fahari yetu unaendeshwa na Idara ya Utamaduni na Utalii iliyo ndani ya kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.

Kutokana na taaluma kubwa iliyonayo katika utafiti, urithi wa utamaduni na utalii, timu ya chuo kikuu cha Iringa inaratibu na kusimamia mradi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwajibika kwa mfadhili.

Dkt. Jan Kuever

Mkurugenzi Mtendaji

Tangu kufuzu masomo yake ya Shahada ya Uzamili (M.A) katika masuala ya Anthropolojia na Utamaduni nchini Ujerumani mwaka 2007, Dkt. Jan Kuever anafanya kazi ya uhadhiri na pia katika upande wa utawala katika chuo kikuu cha Iringa.

Yeye ni mwandishi na mwanzilishi wa mradi wa fahari yetu na pia ndiye meneja wa Mradi ambaye anajukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazohusu mradi.

Dkt. Kuever pia alitumia mradi wa fahari yetu kama uchunguzi kifani (case study) katika utafiti  kwa masomo yake ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya masuala ya Urithi na Utamaduni katika chuo kikuu cha  BTU Cottbus-Senftenberg, nchini Ujerumani. Utafiti alioufanya unachunguza kinadharia na vitendo uhusiano  kati ya utamaduni,urithi na maendeleo endelevu.

20160227-105731

Jimson S. Sanga

Meneja Msaidizi

Jimson Sanga ni Mhadhiri katika idara ya Anthropolojia, utamaduni na utalii katika chuo kikuu cha Iringa tangu mwaka 2011.  Mwaka 2014, alihitimu  Shahada ya Uzamili (M.A) ya Utalii, Utamaduni na Jamii.

Sanga anajukumu la kumsaidia Meneja Mradi katika kuratibu na kufatilia masuala yote yanayohusu mradi ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu na kuendeleza shughuli na mawasiliano yote yanayohusu mradi.

Akihusianisha na historia ya utafiti wake alioufanya katika masuala ya Ethnolojia na muziki (Ethnomusicology) moja ya shabaha kuu ya kazi yake ni kufanya muziki na ngoma za asili kuwa bidhaa za kibiashara na zenye faida kupitia utalii.

 

Timu ya Utafiti

Mratibu wa utafiti kwa kushirikiana na  wasaidizi wake  huzalisha maarifa na kufasiri mawazo ya tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia katika kubuni, kukusanya na kuzifanyia maonesho bidhaa mbalimbali zilizopo katika makumbusho (Boma). Ushiriki wa timu hii ya utafiti katika mradi unasaidia kukiendeleza kitaaluma na uwezo chuo kikuu cha Iringa na mkoa kwa ujumla.