Maonyesho hayo yanatoa utangulizi kwa mgeni kuhusu historia ya Mkoa wa Iringa na mkazi wake maarufu, Chief Mkwawa wa kabila la Wahehe.

Mji wa Iringa ulianzishwa mwaka 1896 na wakoloni wa kijerumani kama kituo cha kijeshi walichokiita ‘Iringa mpya’.  Hii ilikuwa baada ya wajerumani kwanza kushindwa na jeshi la Wahehe katika pambano la Lugalo mwaka 1891, na baadae kufanikiwa kubomoa ngome ya Chifu Mkwawa mwaka 1894. Wakazi wa kwanza wa Iringa mpya walikuwa ni askari wa kiafrika pamoja na familia zao, ambao walipigana kwa niaba ya mjerumani.

Iringa ilianguka mikononi mwa waingereza mwaka 1916 wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Chini ya utawala wa kiingereza, mji wa Iringa ilikua taratibu kama sehemu ya kufanya biashara. Ukuaji huu ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwasili kwa wajasiriamali wa Kihindi na Kiarabu, na wakulima wa Kigiriki waliokuja kulima zao la tumbaku. Wagiriki walitoa ajira kwa Wakinga wengi kutoka Makete kwaajili ya kufanya kazi kwenye mashamba yao ambapo hatimaye iliwapelekea kuanza biashara zao wenyewe katika mji wa Iringa.