Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania ili andaa maonesho na kutoa mialiko kwa wadau mbalimbali wa utalii, ikiwemo Mradi wa fahari yetu Tanzania na Makumbusho ya Mkoa Iringa Boma, maonyesho haya yenye lengo la kuwajengea waheshimiwa wabunge uelewa na kuwapatia elimu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, malikale, na uendelezaji wa utalii nchini maonesho yalifanyika katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma kuanzaia tarehe 30 Mei hadi 3 Juni 2024.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angela Kairuki, alipotembelea banda la Makumbusho ya Mkoa wa Iringa Boma, alitoa pongezi za dhati kwa mradi wa fahari yetu Tanzania kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kutangaza na kuendeleza utalii wa kiutamaduni. Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa mradi huu katika kuanzisha na kusimamia makumbusho ya Mkoa wa Iringa, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa taifa letu.

“Nimefurahishwa sana na kazi kubwa mnayofanya katika kutangaza utalii wa kiutamaduni,” alisema Waziri Kairuki. “Nimekuwa nikifuatilia taarifa zenu kupitia mitandao ya kijamii kama Instagram, na ni dhahiri kuwa mnachangia kwa kiasi kikubwa katika kuonyesha uzuri na utajiri wa utamaduni wetu kwa dunia nzima.”

Dkt. Jan Kuver, Mkurugenzi wa Mradi wa Fahari Yetu na makumbusho ya Iringa Boma, anaeleza kuwa, Maonyesho haya yaliyofanyika Dodoma ni jukwaa muhimu la kutangaza utalii wa ndani na nje kwa wabunge na wadau wengine wa utalii. Maonyesho haya yanaweza kuongeza chachu ya kutangaza utalii kwa kuwawezesha wabunge na viongozi wengine kuona na kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utalii, na hivyo kuboresha uelewa na ushirikiano wao katika kuendeleza sekta hii muhimu. Ushirikiano baina ya Wizara ya Utalii na wadau wengine katika maonyesho haya ni wa manufaa makubwa, kwani unawawezesha kubadilishana mawazo na mbinu bora za kutangaza utalii, na hivyo kuleta ubunifu na ufanisi katika sekta hii.

“Kupitia maonyesho haya, sisi kama fahari fetu Tanzania tumejifunza vingi na kupata fursa ya kukutana na wadau wengi ambao tunaweza kushirikiana nao katika kufanya shughuli za utalii”.

Makumbusho ya mradi wa fahari yetu Tanzania unatoa  shukrani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaliko huu muhimu.Kwani umetuwezesha kuelezea shughuli zinazofanywa na makumbusho na kutoa fursa ya kutangaza utalii kwa waheshimiwa wabunge. Tunatumaini kuwa wabunge hawa watakuwa mabalozi wa kutangaza utalii unaopatikana Iringa katika majimbo wanayowakilisha.