Nyanda za juu kusini mwa Tanzania
Nyanda za juu kusini mwa Tanzania ni eneo lililo katika ukanda wa kijiografia wa kusini magharibi mwa nchi ya Tanzania. Ukanda huu unajumuisha mikoa sita ya kiutawala ambayo ni Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma. Eneo hili linaundwa na mkusanyiko wa milima inayotokana na Volcano, misitu na nyasi. Mbali na asilimia kubwa ya vyakula vinavyozalishwa nchini Tanzania kutokea katika ukanda huu, Nyanda za juu kusini pia ni eneo lenye baridi hasa katika mwezi Juni na Julai .
Ukanda huu pia unauzoefu wa kuwa na mvua kubwa zinazonyesha katika vipindi viwili vya mwaka. Eneo la nyanda za juu kusini ni kivutio kikubwa cha utalii likiwa na vivutio mbali mbali likiwemo bonde la ufa ,maziwa, mito, na reli ya TAZARA .
Mkoa wa Iringa
Iringa ni mkoa wa kiutawala uliopo kaskazini mashariki mwa ukanda wa nyanda za juu kusini. Mkoa wa Iringa unakilometa za mraba 35,503 na idadi ya watu 941,238 (Kwa mujibu wa sensa ya idadi watu na makazi ya mwaka 2012). Mji mkuu wa wake (Iringa mjini) ulianzishwa katika miaka ya mwanzo ya karne ya 19 baada ya kumalizika kwa vita kati ya Wahehe chini ya uongozi wa Chifu Mkwawa na jeshi la wakoloni la Kijerumani.
Iringa ni moja ya mikoa yenye vivutio mbalimbali vya kitalii ikiwa pamoja na mbuga za wanyama pori za Ruaha na Udzungwa. Mkoa pia una vivutio vya kihistoria na kitamaduni kama vile eneo la mali kale la Isimila (Isimila Stone Age) na makumbusho ya Mkwawa ya Kalenga. Kufuatia mtaji mkubwa wa kitalii ulionao, mkoa wa Iringa sasa unaendelezwa na serikali na taasisi binafsi na kuwa kitovu kikuu cha utalii katika nyanda za juu kusini Tanzania.