Kwa mara ya tatu mfululizo, Makumbusho ya Mkoa Iringa Boma na Kituo cha Utamaduni yamepokea kwa furaha wanafunzi wapatao mia tatu wa kozi ya Utalii kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma. Ziara hii ni sehemu muhimu ya kujifunza kwa vitendo, ambapo wanafunzi wanapata fursa ya kuongeza ujuzi na maarifa yao ya kitaaluma. Hii ni hatua muhimu katika kuwaandaa kwa mafanikio wanapomaliza masomo yao ya chuo.

Mbali na kukuza taaluma za wanafunzi, ziara hizi pia zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kuhamasisha utalii wa kiutamaduni na utalii wa ndani. Kupitia ziara hizi, tunazidi kuthibitisha kwamba utamaduni wetu ni hazina inayoweza kuwavutia watu wa rika na taaluma mbalimbali, na hivyo kuimarisha ushirikiano baina ya sekta ya elimu na utalii.

Tunatoa shukrani za dhati kwa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuendelea kutuchagua kama sehemu ya mafunzo yao ya vitendo. Makumbusho ya Mkoa Iringa ni kielelezo cha urithi wa kihistoria na kiutamaduni uliopo katika Manispaa ya Iringa. Ushirikiano huu ni wa manufaa makubwa, siyo tu kwa wanafunzi, bali pia kwa jamii yetu kwa ujumla.

Kwa moyo mkunjufu, tunawakaribisha tena kuungana nasi wakati mwingine. Tutaendelea kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu na kukuza uelewa kuhusu utamaduni wetu kupitia utalii wa kiutamaduni. Karibuni tena Iringa, mahali ambapo historia na utamaduni vinaishi milele.